Mrija wa mkojo (urethra) ni njia ya kutolea mkojo nje ya mwili kutoka kwenye kibofu na unapoziba hufanya utokaji wa mkojo kuwa wa tabu na kusababisha maumivu makali sana. Kitaalamu kuziba kwa mrija wa mkojo huitwa urethral stricture na husababishwa na kovu linalotokea katika sehemu ya mrija baada ya mtu kuumia, kufanyiwa upasuaji au kupona magonjwa ya zinaa.
Magonjwa ya zinaa yanayoweza kusababisha kovu kwenye njia ya mkojo yapo mengi na tutayajadili katika matoleo yetu yajayo kwani yapo mengi.
Hivyo ni muhimu sana mtu kutibiwa mapema anapokuwa na magonjwa hayo.
Kuziba kwa mrija huo kunaweza pia kusababishwa na uvimbe karibu na eneo la kinena unaokandamiza mrija.
Wengi wanaopatwa na tatizo hili ni wale ambao wana historia ya kuugua magonjwa ya zinaa au kuwahi kuwekewa mipira ya mkojo au vifaa vya namna hiyo (catheter au cystoscope) sehemu hizo au husababishwa na kuvimba tezi dume (BPH) kwa wanaume.
Wengine wanaopatwa na tatizo hili ni wale wanaokuwa na historia ya kuumia au kupata majeraha maeneo ya sehemu za siri au wanaopata maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa kwenye mrija wa mkojo (urethritis).
Tatizo hili mara nyingi huwakumba wanaume na ni mara chache sana kuwakumba wanawake au watoto wachanga labda wale wanaozaliwa wakiwa na tatizo hili ambapo kitaalamu huitwa congenital urethral stricture.
DALILI.
Mtu mwenye tatizo hili anaweza kuwa na dalili zifuatazo:
⏺kwa mwanaume hutokwa na manii zilizochanganyika na damu.
⏺kukojoa mkojo mweusi au uliochanganyika na damu,
⏺kutoa mkojo kidogo sana tena kwa shida, kukojoa mara kwa mara na kushindwa kumaliza mkojo wote.
⏺Wengine huona dalili za mkojo kujitokea wenyewe, hivyo mhusika kujikojolea, kusikia maumivu wakati wa kukojoa au chini ya tumbo au kwenye kinena, mkojo kutawanyika ovyo wakati wa kukojoa na uume kuvimba.
Mgonjwa aonapo dalili hizo anashauriwa kumuona daktari ili afanyiwe uchunguzi wa mwili na namna anavyokojoa. Uchunguzi wa mwili unaweza kuonesha kupungua kwa mkondo wa mkojo, uchafu kutoka katika mrija wa mkojo, kibofu kilichojaa/kuvimba kwa mitoki ya maeneo ya kinena, tezi dume iliyovimba au yenye maumivu, kuhisi kitu kigumu chini ya uume.
Daktari akiona moja ya dalili hizo mgonjwa anaweza kuchunguzwa kwa vipimo tofauti kama vile kile cha kuchunguza mrija pamoja na kibofu cha mkojo (cystoscopy),kuangalia kiasi cha mkojo kinachobaki katika kibofu baada ya mkojo kutoka, X-ray ya mrija wa mkojo (Retrograde urethrogram) atapimwa kama ana magonjwa ya zinaa kwa kumfanyia uchunguzi wa mkojo (Urinalysis) pamoja na kuotesha mkojo (Urine culture).
USHAURI.
⏺Mgonjwa mwenye tatizo hili atibiwe haraka maana kama tatizo likiachwa linaweza kusababisha kuziba kabisa kwa njia ya mkojo na kusababisha mkojo kujaa katika kibofu, hali ambayo, pamoja na kuleta maumivu makali kwa mgonjwa inaweza pia kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.
⏺Watu wajikinge na magonjwa ya zinaa ambayo yanasababisha tatizo hili na wawe makini na kazik zinazoweza kusababisha kuumia sehemu nyeti na kuzalisha tatizo hili.
Share na mwenzako apate elimu hii pia.
Home »
AFYA
» AFYA YETU - FAHAMU MAGONJWA YANAYOSABABISHA KUZIBA KWA MRIJA WA MKOJO (URETHRAL STRICTURE)
No comments:
Post a Comment